LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wachimbaji madini Songwe waruhusiwa kuendelea na shughuli zao

Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia mbele) na Meneja wa Kiwanda cha chokaa cha Lime Africa kilichopo katika Kata ya Nanyala Wilayani Mbozi Mkoani Songwe, Fredy Msindo (kushoto mbele) pamoja na msafara  wakiendelea na ziara katika eneo la kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa wa Songwe yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Meneja wa Kiwanda cha chokaa cha Lime Africa kilichopo katika Kata ya Nanyala Wilayani Mbozi Mkoani Songwe, Fredy Msindo (katikati) akielezea shughuli zinazofanywa na kiwanda hicho kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo .
Kutoka kushoto Afisa Madini Mkazi katika Mkoa wa Mbeya, Sabai Nyansiri, Afisa Madini kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mbeya, Ndege Bilagi na Afisa Madini anayesimamia wilaya za Songwe na Chunya, Athuman Kwariko wakinukuu maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) katika mkutano wake na wachimbaji wadogo uliofanyika katika kata ya Nanyala wilayani Mbozi.
Sehemu ya wachimbaji wa madini ya chokaa na ujenzi kutoka katika kata ya Nanyala wilayani Mbozi mkoani Songwe, wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani).
Diwani wa Viti Maalum kutoka Tarafa ya Iyula iliyopo Wilayani Mbozi mkoani Songwe, Messiah Swella akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) katika mkutano huo.
Na Greyson Mwase, Songwe
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewataka wachimbaji wa madini  wanaoendesha shughuli zao za uchimbaji wa madini ya chokaa na ujenzi katika  kijiji cha Nanyala kilichopo katika Wilaya ya Mbozi iliyopo mkoani Songwe kuendelea na shughuli zao wakati wakisubiri  suluhu ya  mgogoro baina yao na kiwanda cha saruji cha Mbeya.

Naibu Waziri Nyongo aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza katika mkutano na wachimbaji wadogo  uliofanyika katika kata ya Nanyala wilayani Mbozi mkoani Songwe ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika  mkoa huo  yenye lengo la  kukagua shughuli za uchimbaji wa madini,  kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

Katika ziara yake Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Songwe, John Palingo, Afisa Madini Mkazi katika Mkoa wa Mbeya, Sabai Nyansiri, Afisa Madini anayesimamia wilaya za Songwe na Chunya, Athuman Kwariko, Afisa Madini kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mbeya, Ndege Bilagi, vyombo vya ulinzi na usalama vya wilaya pamoja na waandishi wa habari.

Nyongo alifafanua kuwa, awali maelekezo yalitolewa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ya kutaka viongozi kutoka katika mikoa ya Mbeya na Songwe kukaa pamoja na kuhakikisha wanamaliza mgogoro wa ardhi kati ya  wakazi wa Songwe na Mbeya na kiwanda cha kuzalisha saruji nje ya mahakama jambo ambalo linafanyiwa kazi kwa sasa.

Alielekeza viongozi kutoka katika mikoa husika kuhakikisha wanashughulikia mgogoro wa ardhi kati ya mikoa miwili na kiwanda cha saruji cha Mbeya kwa wakati huku wananchi wanaojishughulisha na shughuli za uchimbaji madini wakiendelea na shughuli zao kama kawaida katika maeneo husika.

Aliendelea kusema kuwa, jukumu kuu la Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini ni kuhakikisha wanatoa leseni za uchimbaji wa madini kwa kuzingatia sheria na kanuni za madini na kusisitiza kuwa leseni ya uchimbaji wa madini ni tofauti na  hati ya ardhi kwa kuwa inahusisha madini yaliyopo chini ya ardhi.

“Ningependa ieleweke kuwa, leseni ya madini inampa mtu kibali cha kuchimba madini yaliyopo chini ya ardhi ambayo ni tofauti na hati ya ardhi, hivyo wachimbaji wa madini wana haki ya kuendelea na shughuli za uchimbaji wa madini wakati suala la mgogoro wa ardhi likiendelea kushughulikiwa na mamlaka husika,” alisisitiza Nyongo.

Akielezea taratibu za kuchimba madini mara baada ya kupata leseni, Naibu Waziri Nyongo alisema mara baada ya mchimbaji kupata leseni ya uchimbaji wa madini anatakiwa kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na baadaye kutambulishwa katika Ofisi ya Kijiji ili kukutanishwa na wananchi na kufanya makubaliano ya ulipaji fidia kabla ya kuanza shughuli rasmi za uchimbaji wa madini.

Alisisitiza kuwa, ni lazima wawekezaji wote katika shughuli za uchimbaji wa madini kuhakikisha kuwa wanajitambulisha na kufanya makubaliano na wananchi kabla ya kuanza rasmi kwa uchimbaji wa madini ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Nyongo aliwataka maafisa madini katika mikoa ya Mbeya na Songwe kuendelea na zoezi la kuainisha maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini ikiwa ni pamoja na utoaji wa leseni ili uchimbaji wao uweze kuleta tija kwenye uchumi wa nchi.

Aidha, aliongeza kuwa katika maeneo ambayo ni ya hifadhi au vivutio vya utalii leseni zake zifutwe ili kuhakikisha rasilimali za maliasili zinalindwa na kuongeza pato kwenye uchumi wa taifa.

Wakati huohuo Nyongo aliwataka wachimbaji wa madini kuhakikisha kuwa wanalipa kodi mbalimbali  ili fedha hizo ziweze kutumika katika  uboreshaji wa huduma nyingine za jamii kama vile elimu, afya, miundombunu ya barabara.

Pia, Nyongo aliwataka wachimbaji wa madini kuorodhesha kodi na tozo mbalimbali ambazo wanaona ni nyingi na kuziwasilisha katika Wizara ya Madini, ili Wizara iangalie namna ya kuzipunguza na wapate faida zaidi kwenye uchimbaji wa madini.

Awali wakizungumza katika nyakati tofauti wachimbaji hao walieleza changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na mgogoro wa ardhi baina yao na  kiwanda cha saruji cha Mbeya, uharibifu wa mazingira unaofanywa na baadhi  ya wachimbaji na ukosefu wa maeneo kwa ajili ya uchimbaji wa madini.

No comments:

Powered by Blogger.