LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mgodi wa Dhahabu Geita kuanza kusaidia matibabu ya majeraha ya Moto

Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa GGM, Brad Cato akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga wagonjwa walioungua moto.
Mkuu wa Wilaya Geita, Mhe. Josephat Maganga akizungumza na wagonjwa waliofadhiliwa na mgodi wa dhahabu Geita. Wanaoshuhudia tukio hilo ni Meneja anayeshughulikia Jamii na Miundo Mbinu, Manace Ndoroma (kushoto), Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa GGM, Brad Catto (wa pili kulia) pamoja na Meneja anayeshughulikia Afya, Mazingira, Usalama na Mafunzo Dkt. Kiva Mvungi (wa kwanza kulia).
Hafla ya kuwaaga wagonjwa waliopata majeraha ya moto kwa ajili ya kwenda kupata matibabu.
Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) umetumia Jumla ya Shilingi milioni 40 kwa ajili ya kuwagharamia upasuaji wagonjwa 40 walioathirika na ajali za moto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwanza, Sekou Toure.

Mwandishi Maalum
Akizungumza mjini Geita kabla ya kuwasafirisha wagonjwa hao wakiwamo watoto, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa GGM, Brad Cato alisema kwa miaka 17 sasa wakishirikiana na wataalamu wa afya kutoka Australia wa Shirika la Rafiki Surgical Mission wamekua wakitoa tiba hiyo bila malipo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Josephat Maganga alisema Serikali inashirikiana na GGM kupitia mfuko maalumu wa huduma za kijamii (CSR) katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa nia ya kutatua changamoto zinazokumba jamii.

“Kupitia fedha za CSR, changamoto mbalimbali zimeweza kutatuliwa zikiwemo ujenzi wa zahanati, barabara na pia tiba za wagonjwa”. Alisema.

Pia alisema tiba ya upasuaji ina gharama kubwa ambayo ni zaidi ya Sh milioni moja hivyo msaada huo umeokoa maisha ya wananchi wengi ambao kama wasingetibiwa wangeteseka na maumivu.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa GGM, Dk. Kiva Mvungi alisema kwa miaka iliyopita GGM imekuwa ikisaidia watoto na watu wazima wenye midomo sungura lakini kutokana na idadi yao kupungua kila mwaka ndipo walipoanzisha huduma ya kuwasaidia walioathirika na makovu ya kuungua na moto.

“Kampuni yetu kwa kushirikiana na Serikali tumekuwa tukisaidia wagonjwa kila mwaka na awamu hii ni wale walioathirika na kuunguzwa na moto kutokana na idadi ya waathirika wa midomo sungura kupungua”. Alisema.

Pia alisema tatizo la mdomo sungura hutokea pale mama mjamzito anapokosa madini na virutubisho mbalimbali mwilini ikiwamo ukosefu wa madini ya “folic acid”.

Mmoja wa wanufaika wa tiba hiyo, Margareth Damian alisema amekuwa akiishi maisha ya kunyanyapaliwa katika jamii anayoishi huku wakimbatiza majina mengi ya kumbeza.
Alisema alipata makovu hayo mwaka 2014 baada ya kulipukiwa na jiko la mafuta ya taa akiwa Shule ya Sekondari Bariadi.

“Nimekuwa nikiishi maisha ya huzuni kwa sababu pale ninapoishi nimeshabatizwa majina mengi yakiwemo sura mbili, nashukuru sana kwa msaada huu nina imani majina hayo yatakoma”. Alisema huku akitokwa na machozi.

No comments:

Powered by Blogger.