Kampuni ya Acacia yagharamia matibabu kwa wahanga wa matukio ya moto
Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Matangazo.
Baadhi ya
watoto na wazazi wakiwa katika hospitali ya mkoa Mwanza, Sekou Toure wakisubiri
huduma ya upasuji majeraha na kurekebishwa viungo vilivyoshikana baada ya
kupata ajali mbalimbali ikiwemo moto.
Judith Ferdinand, BMG
Wahanga 55 wa matukio ya ajali ikiwemo kuungua kwa moto wameanza kupata
huduma ya upasuaji wa makovu pamoja na kurekebisha viungo vya miili yao vilivyoshikana kutokana na matukio hayo, katika Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa Mwanza Sekou Toure.
Huduma hiyo
inatolewa kwa wahanga hao wakiwemo watoto kutoka maeneo jirani yanayozunguka
migodi ya kampuni ya Acacia ambayo ni North Mara, Bulyanhulu pamoja na Buzwagi.
Akizungumza na wanahabari, Afisa Mahusiano kampuni ya Acacia, Christina Deus alisema wahanga
hao wamekuwa wakipata changamoto ya kutengwa katika jamii baada ya kupata
majeraha ya moto, uji na chai hivyo huduma hiyo itawasaidia kuimarisha hali zao
na kuendelea na shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Alisema
huduma hiyo inatolewa na kampuni ya Acacia kwa kushirikiana na Hospitali ya
Sekou Toure pamoja na Madaktari kutoka taasisi ya Rafiki Surgical Mission ya
nchini Australia na kwamba huduma hiyo inagharimu zaidi ya shilingi Milioni 79.
Deus alisema
huduma hiyo ni muhimu kwa wahanga hao kutokana na wengi wao kutokuwa na uwezo
wa kumudu gharama za matibabu hivyo alitumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi
kujitokeza ili kupata matibabu bure.
Naye Mganga
Mfawidhi Hospitali ya Sekou Toure, Dkt. Bahati Msaki alisema kuna kambi maalum ya siku kumi kuanzia Oktoba 15 hadi 24 mwaka huu hospitalini hapo kwa ajili ya
watu walioungua na moto, maji, uji na chai ambao walitibiwa lakini makovu
katika miili yao hayakuisha pamoja na baadhi ya viungo kama miguu kushikana
hivyo wananchi wajitokeze kupata bure huduma hiyo ya upasuaji kuondoa makovu
hayo pamoja na kutenganishwa viungo vilivyoshikana.
“Jumla ya
madaktari bingwa saba wamejipanga kutoa huduma hii ya upasuaji wa makovu ya
moto na viungo vilivyoshikana ambapo watatu wanatoka Australia, watatu wengine
hapa Sekou Toure na mmoja anatoka Hospitali ya Taifa Muhimbili”. Alibainisha
Dkt. Msaki.
Wazazi ambao
watoto wao wamefika katika Hospitali ya Sekou Toure walitoa shukurani zao kwa
kampuni ya Acacia kwa kuwasaidia kupata huduma hiyo bure.
“Baada ya
mtoto wangu kuungua alipatiwa matibabu lakini makovu hayakuisha ambapo
nilishindwa kugharamia matibabu zaidi hivyo nimefarijika Acacia kutusaidia
gharama za matibabu haya”. Alisema Geofrey Nayinda, mkazi wa Kakola mkoani
Shinyanga.
Tazama BMG Online TV hapa chini
No comments: